Heart Team Africa Foundation

Heart Team Africa Foundation

In the joy of others lies our own

19 Oct

JKCI na HTAF Wazindua Shindano la Insha Mashuleni Kuhusu Magonjwa ya Moyo

Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), kwa kushirikiana na Heart Team Africa Foundation (HTAF), wamezindua shindano maalum la uandishi wa insha kwa shule, likiwa na lengo la kuelimisha na kuongeza uelewa kwa wanafunzi kuhusu magonjwa ya moyo na mishipa ya damu. Shindano hili ni sehemu ya mradi wa miaka mitatu unaojulikana kwa kauli mbiu “Moyo wangu, Afya yangu”, ambao unalenga kujenga msingi wa kinga dhidi ya magonjwa ya moyo kwa watoto na vijana walio katika umri wa shule. Kupitia mradi huu, wanafunzi watafundishwa kuhusu njia bora za kuishi maisha yenye afya, na umuhimu wa kutunza moyo kuanzia wakiwa wadogo. Shindano hili litawashirikisha wanafunzi wa kidato cha 1 hadi cha 6, na litatekelezwa kwa kutumia mbinu mbalimbali za kielimu, ikiwemo kuanzisha vilabu vya afya mashuleni, kusambaza vipeperushi, vijarida, na mabango ya elimu, kuandaa midahalo pamoja na mashindano ya uandishi wa insha. Muda wa kutuma insha umewekwa rasmi kuanzia 8 Oktoba hadi 1 Novemba 2025, na wanafunzi wanahimizwa kushiriki kwa wingi ili kupata nafasi ya kujifunza na pia kushinda zawadi mbalimbali. Zawadi kwa washindi ni kama ifuatavyo: Mshindi wa Kwanza: TSh 3,000,000 pamoja na cheti Mshindi wa Pili: TSh 2,000,000 pamoja na cheti Mshindi wa Tatu: TSh 1,000,000 pamoja na cheti Mshindi wa Nne: TSh 500,000 pamoja na cheti Mshindi wa Tano: TSh 300,000 pamoja na cheti

recent news