Heart Team Africa Foundation

Heart Team Africa Foundation

In the joy of others lies our own

10 Sep

Heart Team Africa Foundation (HTAF) Yatoa Elimu ya Magonjwa ya Moyo Mashuleni Kama Sehemu ya Programu Endelevu

Dar es Salaam, Tanzania – Katika kuendeleza juhudi zake za kuboresha afya ya moyo kwa jamii, shirika lisilo la kiserikali la Heart Team Africa Foundation (HTAF) limeendelea kutoa elimu ya afya ya moyo katika shule mbalimbali nchini. Zoezi hili ni sehemu ya programu endelevu inayolenga kuongeza uelewa wa magonjwa ya moyo kwa wanafunzi na walimu, sambamba na kuhamasisha mitindo bora ya maisha kwa ajili ya kuzuia magonjwa hayo. Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Dr. Adelphina Ncheye, ambaye ni Mkuu wa Programu na Maendeleo ya Biashara wa HTAF, elimu hiyo inajumuisha mada muhimu kama vile: Lishe bora kwa afya ya moyo, Umuhimu wa kufanya, mazoezi ya mwili mara kwa mara, Madhara ya matumizi ya tumbaku na unywaji wa pombe "Wanafunzi wanapewa nafasi ya kuuliza maswali, kushiriki mijadala, na kujifunza kupitia njia shirikishi ili kuhakikisha wanaelewa vyema maudhui yanayowasilishwa," alisema Dr. Ncheye. Akizungumza zaidi kuhusu malengo ya mradi huo, Dr. Ncheye alieleza: "Lengo letu ni kuwafikia watoto na vijana mapema ili kuwajengea msingi imara wa afya bora. Tunaamini kwamba kuwekeza katika elimu ya afya mashuleni kutasaidia kupunguza mzigo wa magonjwa ya moyo nchini katika siku zijazo." Programu hii imepokelewa kwa shangwe na pongezi kutoka kwa walimu na wanafunzi, ambao wameeleza kuwa elimu hiyo ni muhimu sana na inapaswa kuendelezwa kwa mfululizo. HTAF imedhamiria kupanua wigo wa kampeni hii kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa sekta ya afya, elimu na maendeleo ya jamii, ili kuhakikisha kwamba elimu ya afya ya moyo inawafikia watoto na vijana wengi zaidi katika mikoa yote ya Tanzania.

recent news