Heart Team Africa Foundation

Heart Team Africa Foundation

In the joy of others lies our own

23 Aug

MKURUGENZI WA HTAF DKT. MAJANI ASHIRIKI MATEMBEZI YA MAADHIMISHO YA MIAKA 10 YA JKCI

Dar es Salaam, Agosti 23, 2025 — Mkurugenzi wa Heart Team Africa Foundation (HTAF), Dkt. Naizihijwa Majani, ameshiriki katika matembezi ya hiari yaliyoandaliwa na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), ikiwa ni sehemu ya mfululizo wa matukio maalum yanayoelekea kilele cha maadhimisho ya miaka 10 tangu kuanzishwa kwa taasisi hiyo. Matembezi hayo, yaliyofanyika jijini Dar es Salaam, yalikutanisha wadau mbalimbali wa sekta ya afya, wawakilishi wa taasisi za kijamii, pamoja na wananchi, yakiwa na lengo la kuhamasisha jamii kuhusu afya ya moyo na umuhimu wa mazoezi kwa ustawi wa afya kwa ujumla. Mgeni rasmi katika tukio hilo alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mheshimiwa Albert Chalamila, ambaye alipongeza JKCI kwa mchango wake mkubwa katika kuboresha huduma za matibabu ya moyo nchini. “JKCI imekuwa nguzo muhimu katika utoaji wa huduma za kibingwa za matibabu ya moyo. Tuna kila sababu ya kusherehekea mafanikio haya na kuendelea kuunga mkono juhudi za taasisi hii,” alisema Mhe. Chalamila. Kwa upande wake, Dkt. Majani aliipongeza JKCI kwa mafanikio iliyoyapata katika kipindi cha miaka 10 na kusisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya taasisi mbalimbali za afya nchini ili kuongeza wigo wa huduma bora kwa Watanzania. “Ni faraja kushuhudia hatua kubwa iliyopigwa na JKCI katika kipindi kifupi. HTAF itaendelea kushirikiana na taasisi kama JKCI katika kuhamasisha na kuboresha huduma za afya, hasa kwa magonjwa yasiyoambukiza kama ya moyo,” alisema Dkt. Majani.

recent news